Pages

Mwongozo Wa Damu Nyeusi Part 1


 MKE  WANGU


                             Hadithi hii inaanza wakati ambapo msemaji alikuwa anachaguliwa mke atakayeoa na wazee wake lakini hakutaka hivyo yeye alimtaka motto mbichi ambaye angemvumbika mpaka aive. Pia alimtaka mke ambaye alikuwa na sifa ambazo angetaka mke wake awe nazo. Alimweka Aziza rohoni mwake kwani alikuwa kinyume na wasichana ambao walikuwa wamesoma. Alikwa amesoma skuli akapata kuwa mjuaji sana. Msemaji anasema kuwa alipomaliza masomo yake ya juu,mamake alianza kumshawishi  kuhusu mambo ya ndoa. Mama alimtajia wasichana kadhaa lakini aliwakataa wote  na kusema kwamba alimtaka Aziza aliamua kumwoa.
        Baada ya harusi na sherehe walienda fungate yao ambapo msimulizi alipata kumsoma Aziza  na apate kumsomesha. Katika harakati ya kumsoma Aziza,msimulizi aliona kwamba Aziza hakuwa na mazungumzo pamoja naye ,pia aliona jinsi alivyokuwa akimtazama kwa unyarafu. Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo,alisema kuwa alimsikitikia kwani alimwona kama gumegume tu wala si mume wake  kwa sababu hakuwa anafanya kazi yoyote isipokuwa kutembea tembe.
       Aziza aliteta pia kwamba mumewe alikuwa na mikono laini kiasi cha kuwa angemguza mwanamke hangehisi chochote. Aziza hakuwa anavalia viatu kila alipokwenda, na alipoulizwa mbona havalii alisema kwamba hataki kutegemea ngozi za ng’ombe aliyekufa .
     Msimulizi anasema kwamba  humwamrisha mkewe atakavyo kutamshinda. Pia anasema kuwa anaona fedheha kuu,kwanialio  kisonoko ambaye hangeweza kutoka  naye  mbele za watu  alishangaa  jinsi atakavyoishi  naye mbele za watu. Alishangaa jinsi atakavyoishi naye kwa sababu hata mambo madogo ambayo ni muhimu hatilii maanani.
    Aziza alikuwa amenunuliwa brushi ya meno na dawa ya meno lakini hakuvitumia hata kidogo.Aliamua kumuuliza asili yake.
    Msimuluzi alipomuuliza kwa nini hakutumia brushi Aziza alisema kwamba ana mswaki  wake binafsi ambao ulikuwa  umetengenezwa  na mnazi na ndani mlikuwemo unga uliokaa kati kati baina ya jivu na masizi. Aziza alisema kuwa hatautia mswaki ule mdomoni ati kwa sababu  na manyoya ya nguruwe. Pia alisema kuwa wanaotumia brashi baada ya miezi matatu ama mitano huenda kumwona daktari wa meno.
     Siku hiyo, Seluwa mtoto wa shangazi yake aliwatembelea. Wazee wa msimulizi walitaka amwoe Seluwa lakini alimkataa kwa sababu zake. Seluwa na Aziza walikuwa wakitaniana ‘mke mwenzangu’ na pengine ‘wifi yangu’. Wakiwa katika mazungumzo yao Aziza alismskia Bazazi wa madafu akipita huko nje. Msimulizi alimpa Aziza shilingi mbili akanunue hayo,kasha Aziza akamwita Bazazi huyo aende nyumbani mwao.
Bazazi huyo alipofika humo, Aziza akamwambia bwanake kwamba nia ya kumwita huko nyumbani ilikuwa ili aone kuwa alitaka bwana kama huyo. Hayo  ni kwa sababu daima alikuwa anafikiri kazi tu. Baada ya kumwambia hayo,Aziza alimwambia bwanake aampe talaka yake.

2.    Wahusika
Hadithi hii ya Mke Wangu ina wahusika wafwatao;
Msimulizi
Aziza
Fedhele Salim
Salma
Seluwa
Wazazi wa msimuliza
Wahudumu wa msimulizi k.v Mapanya
MSIMULIZI
Msimulizi ni mhusika mkuu katika hadithi. Alizaliwa katika familia ya kitajiri kama anavyotueleza katika ukurasa wa 18.. Ni kijana wa kisasa na mumewe Aziza.
Ni mtamaduni kwa sababu anautii utamaduni wa jadi unaompendelea mwanamume.
Yeye ni msomi aliyesoma hadi viwango vya juu vya elimu.
Aidha, msimulizi anaweza kuelezwa kama mzembe kwa sababu hataki kujihusisha na kazi za sulubu kama vile kuangusha nazi, kuchoma na kuuza mihogo pamoja na kazi nyinginezo. Anashangazwa na uamuzi wa mkewe wa kutotaka kufuliwa nguo wala kuooshewa vyombo.
Ingawa tumemtaja kama mtamaduni, Msimulizi anaweza kueleweka kama mwanausasa kwa sababu anampendekezea mkewe kutenda mambo ya kileo kama vile kuvaa viatu na kupiga mswaki. Kwa sababu hii, anadhihirisha tabia ya mtu asiye na msimamo dhabiti. Ukosefu huu wa msimamo unamfanya ashindwe kujiamulia mambo muhimu maishani kama vile; mke wa kuoa, kazi ya kufanya na namna ya kuiongoza familia yake changa. Kwa maneno  mengine, msimulizi ni mhusika aliyekengeuka na asiyejifahamu.
Isitoshe, msimulizi ni mvumilivu na mwenye subira kwa vile si mwepesi wa kutibukwa na hisia tunadhihirishiwa kuwa anamvumilia Aziza kama mkewe licha ya fedheha anayoipata mbele ya wageni wao wenye ustaarabu wa kimjini. Licha ya Aziza kumdharau, kumwita gumegume na kumsuta kwa kutofanya kazi maishani, msimulizi haonyeshi kuudhishwa na mkewe.
Badala yake, msimulizi anamkubali na kumvumilia mkewe akitaraji kuwa siku moja atazinduka na kuukumbatia usasa na ustaarabu. Aziza anafikia kiasi cha kumwita bazazi wa madafu kasrini mwao, kumsifu bazazi wa madafu mbele ya mumewe na hata kumuomba mumewe talaka. Msimulizi haonyeshi kukasirishwa na maudhi haya yote.
Ni mwenye taasubi ya kiume; hulka hii inadhihirishwa pale ambapo anatarajia kumpata mke ambaye hakwenda skuli. Nia yake ni kumpata mke ambaye hatakuwa katika ngazi moja ya kielimu naye. Tunaweza kuhitimisha kuwa msimulizi hataki mwanamke mwenye ung’amuzi wa usawa wa kijinsia na haki za wanawake. Kwa  mujibu wake, matatizo ya ndoa hutokana na midomo na ujuaji wa wanawake.
Aidha, anapanga kumvinya mkewe na kumfunza mambo ya kisasa ya uanagenzi. Anammithilisha mkewe na tunda linalohitaji kuvinywa. Anaonyesha dharau kwa wanawake kwa sababu anawalinganisha na watoto wadogo ambao hawaachi kisebusebu (uk. 21)
Umuhimu wa msimulizi
Msimulizi ni mhusika mkuu katika hadithi hii. Anaakilisha kizazi kilichochanganyikiwa. Kizazi kilichojipata katika nja panda, yaani katikati ya ukale na usasa.
Mbali na kuchanganyikiwa, msimulizi anaakilisha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii ya kisasa kama vile mfumo mbaya wa elimu inayolenga ajira, ukosefu wa ajira, ujuma na uzembe, matatizo ya ndoa na kadhalika.
Msimulizi ni kielelezo cha jamii ambayo inashindwa kuyaelewa mazingira yake. Anashindwa kuuelewa utamaduni wake, mahitaji yake majukumu yake, na hata hamwelewi mkewe.
Waama, ni kupitia kwa mahusiano ya Msimulizi na mkewe ndipo tunabaini kuwa elimu na hekima ni mambo mawili tofauti.

AZIZA
Ni mhusika mwingine ambaye anaweza kuutajwa kama mhusika mkuu. Ni mkewe msimulizi. Tofauti na msimulizi, Aziza alizaliwa na kukuzwa shamba.
Aziza ana sifa zifwatazo;
Kwanza, Aziza ni mdadisi wa mambo. Anamchuja msimulizi na kuugundua udhaifu wake. Ni kutokana na udadisi huu ndipo anagundua kuwa yeye na msimulizi wako na mawazo yaliyobaidika.
Anaumaizi ulelemama wa mumewe wa kutofanya kazi na tabia ya kutegemea wazazi wake. Anadadisi na kugudua viungo vya dawa ya meno; tumbawe, sabuni na arki za peremende kali. Pia, anagundua kuwa mswaki si lolote si chochote bali nywele za nguruwe.
Aziza anaweza kuelezwa kama mhafidhina, anayapinga madai ya msimulizi kwamba riziki ya kazi imekosekana. Yeye anashikilia kuwa mtu hawezi akakosa kazi ulimwenguni, kazi anazozitaj ni kazi za jadi kama vile kuangusha nazi, kuchoma na kuuza mhogo na hata kuchunga punda. Uhafidhina wa Aziza unazidi kujiidhihirisha pale anapokataa katakata kuvaa viatu huku akishikilia kukanyaga chini kote aendako. Anawadharau wanaume wa kimjini enye usasa na mwishowe anajiafadhalisha kuolewa na mwanamume wa shamba.
Mwenye dharau; kila mara, Aziza anamchuja mumewe kwa dharau. Anavidharau viatu, mikono ya mumewe, mswaki na dawa ya meno ya kisasa. Kitendo cha kumsifia bazazi wa madafu mbele ya msimulizi pia ni ishara ya dharau.
Sifa nyingine ya aziza ni kuwa yeye ni mwenye hekima, majibizano yake na mumewe yanadhihirisha hekima tele. Anashangaa ni kwa nini walishwe na wazazi wa msimulizi. Anaumaizi udhaifu uio kwenye dawa ya kisasa ya meno, anashangaa ni kwa nini wale waliotumia dawa ya meno waliyang’oa meno yao kila wakati. Hekima hii inamfanya msimulizi kukiri kuwa mkewe ni mtu asiyeweza kupatwa kiotoni.
Mwenye msimamo thabiti; Aziza anadhihirisha kuwa na msimamo thabiti kwa mambo anayoyaamini. Anakataa kushawishiwa kuukumbatia usasa. Anashikilia na kuyaishi maisha ya jadi hata kama kila mtu aliye karibu naye ameukubali usasa.
Anapojibizana na mumewe, Aziza anajitokeza kama mhusika jasiri. Anakataa kuwekwa chini na mumewe. Hali ya kutopata masomo ya kisasa haimnyimi uasiri wa kuaimama kidete na kuyatoa mawazo yake. Kutokana na ujasiri wake, anamkabili mumewe na kuzishutumu tabia zake bila hofu wala woga. Hatimaye, anamjulisha msimulizi kimasomaso kuwa angetaka apewe talaka yake.
Umuhimu wa Aziza
Aziza amechorwa kama mhusika bapa sugu. Anao msimamo sugu kuhusu utamaduni wa jadi na hakubali kuubadili msimamo huu.
Anawakilisha watu wanaoshikilia msimamo thabiti wa kuutetea ujadi. Aziza anaweza kutazamwa kama mdomo wa mwandishi kwa sababu mwandishi amempa hekima nzito na amewezeshwa kumpiku msimulizi katika migogoro yao mbalimbali.
Aidha, aziza ametumiwa na mwandishi kuutetea utamaduni wa waafrika dhidi ya athari za kigeni kama vile elimu na mavazi.
Aziza ametumiwa kupitisha ujumbe kuwa furaha na utu wa mtu si elimu wala utajiri wala ajira, bali maadili mema, bidii, heshima na mapenzi ya dhati.
Kupitia kwa Aziza, tunajuzwa kuwa mwanamke wa kiafrika amejikomboa kimawazo na anaweza kujifanyia maamuzi tofauti na adhaniwavyo na wanaume wenye taasubi za kiume kama msimulizi.
Maswali
1.      Jadili uhusika (hulka na umuhimu) wa msimulizi na wa Aziza
2.      ‘Msimulizi na mkewe hawapatani kwa lolote’, jadili kauli hii ukirejelea hadithi fupi ya Mke Wangu.
FEDHELE SALIM, SALMA NA SELUWA wanaweza kuelezwa kama wasichana wa kisasa; msimulizi anawataja kama wasichana waliojaa utamaduni wa kisasa.
Fedhele anaelezwa na msimulizi kama msichana msomi. Ingawa hivyo, tabia yake ya kuvalia kanzu fupi na kuandamana na wanaume hazimpendezi msimulizi.
Salma anadhihirika kama msichana mwenye kujipodoa na marangi ya mashavu na midomo.
Msimulizi anatueleza kuwa Seluwa ana ‘kidomo’ yaani, ni mtu wa kuongea maneno mengi. Isitoshe, katika uk. wa 24, anamtaja Seluwa kama msichana mwenye kujipodoa na kupendeza.anamtaja kama mwingi wa bashasha, mizaha na furaha.
Umuhimu wa Fedhele, Salma na Seluwa
Hawa watatu ni wahusika wasaidizi.
Wanatusaidia kumwelewa msimulizi kwa sababu wanatusaidia kujua ni mambo gani yasiyompendeza msimulizi.
Aidha, sifa zao zinakinzana na za Aziza hivyo basi wanatusaidia kujua hulka za Aziza.
WAZAZI WA MSIMULIZI ni wakwasi kwa sababu msimulizi anatueleza kuwa yeye alizaliwa katika familia ya kitajiri.
Wao ni wahifadhina kwa sababu wanamlea mtoto wao kwa kuongozwa na tamaduni za jadi za kiafrika na hata wanamchagulia mke kwa mujibu wa kaida za jadi za kiafrika. Msimulizi anatueleza kuwa, …wazee wangu, juu ya utajiri wao, hawakupenda kubadili mila zetu… (uk. 18)
Mamake msimulizi anadhihirisha hekima anapomwongoza msimulizikumchagua na kumwoa Aziza. Anapendekeza wasichana ambao anajua msimulizi hatakubali kuwaoa.
Umuhimu wa wazazi wa msimulizi
Wazazi wa msimulizi ni wawakilishi wa utamaduni wa jadi.
Maswali
1.      Jadili uhusika wa msimulizi na Aziza
2.      Je, Seluwa, Salma na Fedhele Salim wana umuhimu gani katika hadithi
3.      Unadhani ni kwa nini mwandishi akatumia anwani ya mke wangu
4.      Ni vipengele vipi vya utamaduni wa jadi anavyovipendelea mwandishi.

3.    DHAMIRA
Yaelekea kuwa mwandishi ana nia ya kutubainishia kuwa Elimu ya jadi ni bora kuliko mafunzo ya kisasa ya shuleni na vyuoni; hili linabainika tunapoona Aziza akipewa sifa ya kuwa mpevu wa hekima nzuri na mwandishi.
 Msimamo wa mwandishi ni kuwa watu wa shamba waolewe na wenzao wa shamba na wale wa mjini waolewe na wale wa mjini. Msimamo huu umetokana na yale anayoyaona katika jamii; migogoro katika ndoa, ubaidi wa kifikra utabaka na mitazamo ya maisha inayokinzana.
Yamkini wimbi la kisasa ambalo limeiacha jamii ya kisasa katika njia panda limemchochea mwandishi kuiandika hadithi hii ili awakumbushe watu kurejelea kaida zao za jadi.
4.    MAUDHUI
Mafunzo yafwatayo yanajitokeza katika hadithi ya Mke Wangu.
·         Utamaduni
·         Usasa na mabadiliko ya kijamii
·         Elimu
·         Utabaka, utengano na mitafaruku
·         Ndoa
·         Taasubi ya kiume na matatizo yanayowakumba wanawake
·         Ukengeushi

1.    Utamaduni
Mohammed Said Abdulla anadhihirisha utamaduni wa aina mbili.
Kuna utamaduni asilia wa Afrika unaoendelezwa na Aziza na bazazi wa madafu. Aziza anaelezwa kama mwenyeji wa shamba. Aidha anatetea na kudumisha mila za kiafrika kama vile bidii kazini. Anashikilia kuyaishi maisha ya shamba kama vile kutovaa viatu.
Anapuuzilia mbali matumizi ya dawa mswaki na dawa ya meno. Anakataa kuathiriwa na utamaduni wa kisasa.
Utamaduni wa kisasa unaendelezwa nawahusika kama msimulizi, Seluwa, Fedhele na Salma.
Fedhele, Salma na Seluwa wanajipodoa kwa vipodozi na rangi za kisasa.
Msimulizi anatetea uvaaji wa viatu, matumizi ya mswaki wa kisasa na dawa ya kisasa ya meno.
Aidha, msimulizi ni mwanausasa aliyeipata elimu ya kisasa, anaishi kwenye nyumba ya kisasa, anatumia mavazi ya kisasa na vipodozi vya kisasa kama vile kitana.
Selume na msimulizi wanaamkuana kwa kuingiana maungoni; mtindo ambao ni wa kisasa.
2.    Elimu
Elimu ni mfumo wa mafunzo yanayopatikana shuleni, vyuoni au  maishani.
Maudhui ya elimu yameendelezwa kuwili kwenye hadithi ya Mke Wangu.
Kwanza ni yale mafunzo yapatikanayo katika maisha.
Aidha, ipo elimu nyingine inayopatikana vyuoni.
Japo Aziza ni msichana wa shamba, anadhihirisha ukomavu wa hekima. Hii ni ishara tosha kuwa amebobea katikaa mafunzo ya maisha kuhusu maswala ya kazi, ndoa, mahitaji ya jamii na matarajio ya jamii kuhusu wajibu wa mume na mke ndoani.
Msimulizi na Fedhele ni wahusika waliopokea mafunzo ya vyuoni. Wanatajwa kama wahusika waliopokea elimu ya hadi viwango vya juu.
Hata hivyo, elimu hii iliyopokewa na msimulizi inadhihirika kuwa duni kwa sababu haijamwezesha msimulizi kujitegemea. Ni elimu yenye lengo la kupata kazi na wala hailengi kumsaidia mtu kujimudu katika mazingira yake.
Aidha elimu hii inashindwa kumuhami msimulizi na mbinu mwafaka za kuyakabili matatizo ya ndoa. Anashindwa kuidhibiti ndoa yake na Aziza.
Kwa hivyo basi tunaweza kudadavua kuwa mwandishi anaipendelea elimu ya jadi inayompa mtu mafunzo ya maisha dhidi ya ile elimu ya kisasa inayopatikana shuleni na vyuoni.



3.    Utabaka na Utengano
Utabaka ni mfumo wa kijamii unaowagawa watu kwenye makundi kutegemea uwezo wao wa kiuchumi au kijamii.
Kwa upande wake, utengano ni hali ya watu kuwa mbali na wengine. Umbali hiu waweza kuwa wa kiuchumi, kijamii, kijinsia, kimsimamo, kifikra au kimawazo.
Kwenye hadithi ya Mke Wangu, utabaka unajitokeza pale tunapodhihirishiwa utajiri wa wavyele wa msimulizi na wakati uo huo tunadhihirishiwa ufukara wa wahusika wengine kama bazazi wa madafu. Maisha ya bazazi wa madafu nay a msimulizi yanatupa taswra kamili ya utabaka wa kijamii.
Utengano wa kifikra pia unajitokeza kati ya msimulizi na mkewe. Wawili hawa wanaakilisha misimamo pinzani kati ya fikra za jadi na zile za kisasa.



4.    Ndoa
Ndoa ni makubaliano rasmi kati ya mume na mke ya kuishi pamoja.
Ndoa zinazotajwa hadithini ni zile za wazazi.
Ndoa zilizotajwa hadithini ni mbili. Kwanza, ipo ndoa kati ya msimulizi na Aziza. Ya pili ni ndoa kati ya wazazi wa msimulizi.
Ndoa kati ya msimulizi na Aziza inakumbwa na matatizo si haba. Matatizo haya yanachimbuka kutokana na ubaidi wa malezi ya wachumba hawa. Huku msimulizi umuhimu wa vyombo na mienendo ya kisasa, Aziza anasisitiza kuwa mila, desturi na vyombo vya jadi ni lazima vitekelezwe. Ndoa hii inaishia kwa Aziza kumwomba mumewe talaka.
Mwishoni mwa hadithi tunaashiriwa ndoa mpya kati ya aziza na bazazi wa madafu.
Hatuelezwi sana kuhusu ndoa kati ya wazazi wa msimulizi. Hata hivyo ndoa hii inaweza kuelezwa kama ndoa inayoongozwa na kaida za jadi. Hii ni kwa sababu wanamuongoza msimulizi kumuoa mke anayefwata kaida za jadi.


5.      Taasubi ya kiume na matatizo yanayowakumba wanawake
Taasubi ya kiume ni mfumo wa kijamii ambamo mwanamume hupewa nafasi ya juu kumliko mwanamume. Kwenye mfumo kama huu, mwanamume hukumbwa na matatizo si haba.
Jamii ya mke wangu inaweza kuelezwa kama inayoongozwa na mfumo huu.
Msimulizi anabainisha taasubi ya kiume pale ambapo anawalaumu wanawake kwa matatizo yote yanayokumba ndoa. Anapomwona Fedhele na wanaume, anamlaumu fedhele pekee yake na kuwapuuzilia mbali wale wanaume.
Isitoshe, msimulizi anawadharau wanawake na kuwalinganisha na watoto.
Aidha, msimulizi anamlinganisha mkewe na tunda linalostahili kuvimbikwa ili live.
Hata hivyo, japo Aziza ni mwanamke wa shamba, anajitokeza kama mwanamke aliyejikomboa kimawazo na mwenye hekima tele.


6.      Ukengeushi
Ukengeushi ni hali ya mtu kwenda kando na uhalisia wa kijamii. Msimulizi, Fedhele Salma na Seluwa ni baadhi ya wahusika ambao wamekengeuka. Maisha yao hayaingiliani na uhalisia wa mazingira yao.
Japo, fedhele na salma wanajipaka marangi kwa azma ya kuonyesha kuwa wamezinduka, tabia hii inawaudhi wanajamii akiwemo msimulizi. Aidha, tabia ya Fedhele ya kutembea usiku na wanaume inamuharibia sifa mbele ya msimulizi.
Msimulizi naye ni mhusika mwingine aliyekengeuka, licha ya kuwa yeye ni msomi aliyefikia kileleta. Anapigwa chenga na hekima ya msichana wa shamba. Aziza anamdhihirishia kuwa elimu yake haikumfaa kwa lolote bali imechangia kumfumba macho ili asiung’amue uhalisia wa kijamii.
Maswali
Eleza namna maudhui yafwatayo yalivyoendelezwa kwenye hadithi ya Mke Wangu;
i)                    Ndoa
ii)                  Utabaka
iii)                Elimu
iv)                Ukengeushi
5.  MATUMIZI YA LUGHA
Zifwatazo ni baadhi ya mbinu za kisanaa na mbinu za lugha zilizotumiwa kwenye hadithi.
MBINU ZA KISANAA ni mbinu zote zinabuniwa na kutumiwa na msanii kuupitisha ujumbe wake. Hizi ni pamoja na usimulizi, taswira, virejeshi nyuma, maswali balagha, sadfa, chuku, kinaya, hadithi ndani ya hadithi.
MBINU ZA LUGHA pia huitwa tamathali za usemi. Ni matumizi ya vipengele vya lugha vya kimapokeo kama vile methali, nahau, vitendawili, tanakali za sauti, istiari na tashbihi.
1.      Usimulizi uliotumiwa kwenye hadithi ni wa nafsi ya kwanza.
Msimulizi ni mmoja wa wahusika.
Anatusimulia alivyozaliwa na wakwasi, akasoma hadi viwango vya juu na akachaguliwa mke wa shamba na wazazi wake.
Anaendelea kutusimulia kadhia zinazoikumba aila yake na migogoro inayoibuka kati yake na mkewe.
2.      Taswira mbalimbali zinajitokeza kwenye hadithi ya Mke Wangu. Taswira ni picha zinazochoreka mawazoni tunapozisoma kazi za fasihi. Pia huitwa jazanda.
Kutokana na maelezo ya msimulizi, tunapata picha kamili ya Salma, Fedhele na Seluwa. Fedhele na Salma wanachoreka mawazoni mwetu kama wasichana waliojirema na kujipodoa kwa mapambo ya kisasa. Katika ukurasa wa 18, Fedhele anaelezwa kama msichana aliiyevalia kanzu fupi na Salma kama mwenye kujipaka marangi.
Mbali na kuwa mwenye kidomo, Seluwa anachorwa kama msichana mwenye kujipodoa, msichana mcheshi na mwingi wa usasa.
Swali:
Eleza picha inayokujia mawazoni;
Kumhusu msimulizi, Aziza na bazazi wa madafu.
Kuhusu mikono ya msimulizi na nyayo za Aziza.
3.      Hadithi inaanza kwa kirejeshi nyuma. Tunarejeshwa hadi enzi ambazo msimulizi alichaguliwa mke na ninaye. Kirejeshi nyuma hiki ni muhimu katika kuielewa hadithi hii maana kinatupa usuli wa hadithi. Kirejeshi nyuma hiki kinatufafanulia maswala ambayo ni msingi wa migogoro inayoibuka hadithini. Matatizo yanayoikumba familia ya msimulizi yanatokana na vigezo vibovu vilivyotumiwa katika kumchagulia msimulizi mke.
4.      Maswali balagha:
… si lazima kwa hivyo, Aziza awe mwepesi, msikivu, mwelekevu? (uk 18) msimulizi anatumia swali hili kueleza kuwa maadam Aziza kakulia shamba, ni lazima hana jambo. Kwenye ukurasa wa 19, Aziza anatumia maswali balagha kumbeza msimulizi, anauliza;
Mimi nilikuwa nikitazamia nitaolewa na nani katika dunia hii? ...nitapata mume au gumegune tu kama wewe? ...basi wewe ndiye mume wa kunioa miye, we? …huoni wewe wala hupimi?
Katika mazungumzo yake na msimulizi, Aziza anadhihirisha utumizi wa maswali balagha, taja na ufafanue umuhimu wa maswali balagha katika maongezi ya msimulizi. (katika kulijibu swali hili, mwanafunzi atafute na kutaja mifano zaidi ya maswali balagha kwenye hadithi)
5.      Sadfa ni mbinu ya kisanaa ambapo mambo mawili yanatokea kwa pamoja bila kupangwa. Inasadifu kuwa siku ambayo Seluwa alimgeni msimulizi na kumwamkua kwa kumwingia maungoni, bazazi wa madafu anapita akinadi madafu, hapo hapo Aziz anamwita ukumbini, anaomba talaka kutoka kwa msimulizi na kumtaja bazazi wa madafu kama mume wake.

6.      Chuku: ni mbinu ya kisanii inayoeleza jambo kwa namna iliyotiwa chumvi. Katika kuisifia nyayo za miguu yake, Aziza anadai kuwa miguu yake haidungiki kwa miiba. Kwamba hata ukiushindilia mwiba kwenye nyayo zake, mwiba utavunjika!
7.      Kinaya: ni kinaya kuwa msimulizi anayepanga kumchanua Aziza anachanuliwa na Aziza.
8.      Hadithi ndani ya hadithi: kwenye hadithi ya Mke Wangu, msimulizi anaiwazia hadithi ya Nunez ambaye alikuwa chongo na akafikiria kuwa angekuwa mfalme wa vipofu. Hadithi hii inatusaidia kuelewa ung’amuzi wa msimulizi kuwa utamaduni wake na ule wa aziza haungeingiana.
9.      Methali

10.  Nahau na misemo iliyotumiwa hadithini ni pamoja na;
Elekeza rohoni (uk. 18) inayomaanisha kumpenda mtu.
Weka kando inayomaanisha kupuuza
Mtoto mbichi ni msemo wenye maana ya motto mchanga
Tia mguu mjini: pata kufika mjini
Kumvinya mwari: kumwelekeza mtu kwa njia unayotaka wewe
Madarasa: mafunzo
Toa macho: kodoa macho
Zawadi za vicheko: kuchekeshwa
Kumtoa kinyanyaa: kumzindua mtu na kumtoa ushamba

11.  Tanakali za sauti: aliondoka nyatunyatu
12.  Istiara/ istiari
13.  Tashbihi: … kama mtoto anavyonyonya:
…wanawake ni kama watoto wadogo: hii ni kauli ya msimulizi inayotubainishia mtazamo wa msimulizi kuwahusu wanawake.
…ngozi imekacha utafikiri msasa: msimulizi anatumia tashbihi hii kuueleza mkono wa Aziza.


1 comment: