Pages

VITENDAWILI




Mfano kitendawili, utegapo mtegaji

Jibule huwa twawili, wawatatiza majaji

Likawateka akili, waume walo magwiji

Mwisho hutolewa mji, mfumbi kutoshindika

(Boukheit Amana)

Kitendawili ni swali la kiistiari ambapo sehemu moja ya ulingannishi uliopo inadokezwa tu ilhali ya pili inabakia ya kukisiwa. Kama sanaa, vitendawili hutegemea uwezo alionao mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina tofauti katika mazingira yake. Hii ni sanaa inayotendwa (performative) na inayosimama kivyake tofauti na sanaa tegemezi au elekezi (illustrarive) kama methali.
Kitendawili ni kauli inayotenda mawili au inayotendwa na wawili. Ni mchezo wa kuficha maana. Ni utandu wa maneno ambamo dhana husimuliwa kijazanda ili mtu mwingine ang’amue. Vitendawili hulenga maisha ya jamii na shughuli wafanyazo. Vitendawili vingi hushughulikia mambo tofauti yanayomhusu binadamu kama kifo, uhai, chakula, maisha na mazingira.

Asili ya Vitendawili

Vitendawili vina asili mbalimbali
(a)   Mahitaji ya Kisanaa
Kila mtu ana hisia za kisaa ambazo zimefungamana na mazingira. Hisia hizi humfanya mtu kutumia sifa za uumbaji kuyaeleza mazingira hayo. Kwa njia hii mtu huweza kujitosheleza kihisia atoapo kitendawili.
(b)   Mahitaji ya Matumizi
Mtu aliona hoja ya kumwelimisha mwenziwe. Lakini njia ya kumwelimisha haikupatikana. Kwa hivyo aliamua kutumia mazingira yake ya sanaa kuitoa elimu hiyo. Hii ndiyo maana vitendawili vingi hueleza mazingira ambayo ni ya kabla ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.
(c)    Mahitaji ya Kueleza Mazingira na Maendeleo
Mahitaji ya kueleza mazingira na maendeleo ya kisayansi nyakati hizo za zamani kabla ya uvumbuzi na maelezo ya kutosheleza kuwepo. Kwa kuwa mtu alijikuta katika mazingira, ilimbidi atoe maelezo kuhusu mazingira yake. Kwa sababu hii, binadamu alieleza mazingira kwa kutunga visasili vya kuhalalisha kuwepo kwa vitu fulani katika mazingira yake. Kwa mfano kitendawili “Uzi mwembamba umefunga dume kubwa – usingizi”
(d)   Misemo ya Kimtaa
Misemo ya kimtaa itumiwayo na watu wengi katika sehemu fulani. Matumizi ya misemo hii yanapoendelea kupannuka na kupata hadhira kubwa, misemo hiyo hushika kani na kugeuka kuwa vitendawili.

Sifa

Vitendawili hutofautiana kutoka  jamii moja hadi nyingine kwa sababu vitendawili ni zao la utamaduni wa jamii. Licha ya tofauti hizi, vitendawili huwa na sifa zifuatazo ambazo huonekana katika jamii zote:
(a)
    Kuwepo kwa kitangulizi kwa mfano Kitendawili – Tega katika jamii ya Waswahili
(b)
   Matumizi ya lugha ya kiistiari ambapo kitu hulinganishwa na kingine
(c)
    Matumizi ya lugha ya mkato, bila maelezo marefu isipokuwa tu katika vitendawili visimulizi
(d)
   Aghalabu huwa na jibu moja. Hata hivyo vipo vitendawili vichache vya majibu mengi
(e)
    Kufungamana na mazingira ya jamii husika kwa kutaja, kuirejelea na kujifunga kwenye mazingira hayo
(f)
    Kuwepo kwa utaratibu wa kutegua kitendawili chenyewe hasa hadhira inaposhindwa kupata jibu
(g)
    Kuwepo kwa pande mbili za wahusika – mtegaji na mteguaji
(h)
   Maana kueleweka tu katika jamii husika
(i)
     Kuchura taswira kamili ya kinachorejelewa
(j)
     Hadhira kupewa muda kufikiri
(k)
   Kutumia tamathali mbalimbali za lugha

Muundo wa Vitendawili

Muundo ni jumla ya uhusiano unaokuwako kati ya vijisehemu mbalimbali vinavyotengeneza kitu kamili. Katika muktadha wa vitendawili, muundo ni utaratibu unaofuatwa wakati wa kutega na kutegua kitendawili.
     (i)            Kiingizi
Pia huitwa kitangulizi. Hapa mtambaji hutanguliza kwa swali “Kitendawili”. Kifungu hiki hutumiwa kila mara kiasi cha kuwa kama ruwaza fulani. Kitangulizi hiki huwa na umuhimu ufuatao:
(a)
    Kuhanikiza hali ipasayo
(b)
   Kutangaza majilio ya kitendawili
(c)
    Kukatiza yaliyokuwa yakiendelea ili kuwatazamisha hadhira kwenye kitendawili
(d)
   Kuifanya hadhira kuzingatia kitendawili husika
(e)
    Kubainisha mtegaji kwa kumtenga na hadhira
Ifuatayo ni mifani ya viingizi kutoka jamii mbalimbali
Kitangulizi
Kikaribisho
Jamii
Kitendawili
Tega
Waswahili
Kinawia
Njo
Kipare
Namunayi/ Munayi
Kuupa/ Kwitse
Lumasaaba (Uganda)
Kwata ndai
Nakwata
Kamba
Hamne/ Mnaye
Kwithe
Luo
Gwata ndaΔ©
Ndagwata
Kikuyu
Tangoch
Choo
Nandi
Rhipo
Himbiriki
Pokomo
Oyiote
Euo
Maasai
Wata
Nawada
Taita
Getandagwiri
Tega
Abagusii
Chirondoni
Tseka
Duruma
Tangalie
Ega
Digo
Gwata ntai
Ndagwata
Meru
Tukio
Ember
Abasuba
   (ii)            Kikaribisho
Hili ni jibu kutoka kwa hadhira lionyeshalo kukubali kwao kutegewa kitendawili
 (iii)            Mwili
Hapa kitendawili chenyewe hutegwa
  (iv)            Muda wa kufikiri
Hadhira hupewa muda kufikiri na kujaribu kutafuta jibu la kitendawili
    (v)            Kichocheo
Hadhira ikishindwa, tuzo au mji hutolewa kwa mtegaji ili awapatia jibu. Waswahili hutoa mji, Waluo hutoa msichana
  (vi)            Jibu
Jibu hutolewa na mtegaji baada ya kukubali tuzo aliyopewa

Kutegua Vitendawili

Maana na majibu ya vitendawili hutegemea mazingira ya jamii husika. Tupatapo kitendawili kuna uwezekano wa majibu matatu – Kitendawili ni tatizo la kutatuliwa, jibu la sehemu ya kitendawili na na kichocheo baada ya hadhira kushindwa ni sehemu ya kitendawili. Hatua na mambo ya kuzingatia tunapotegua vitendawili ni:
(a)
    Kuelewa kipindi cha wakati kinacholengwa na kitendawili. Kwa mfano kitendawili Baba ana mguu mmoja tu chaweza kuwa na majibu kama Uyoga (jadi) au mwavuli (sasa)
(b)
   Kufahamu mazingira ambamo kitendawili kilitungiwa ili kupata picha kamili ya kitendawili. Kwa mfano kitendawili Mwarabu wangui nimemtuoa biwini kitaeleweka ikiwa mtu ataelewa mazingira ya pwani ambapo jibu ni machicha ya nazi
(c)
    Kuchunguza maana ya maneno. Kitendawili nyumba ya bibi imejaa wapangaji chatubidi kuelewa kuwa wapangaji si watu wa kudumu. Basi maana tupatayo ni kuwa bibi ana chombo anamoweka vitu vya matumizi yake ambavyo havidumu. Jibu ni vijiti vya kiberiti
(d)
   Kuchunguza jinsi linalozungumziwa linafungamana na tabia, picha au umbo la kitu. Kitendawili kipo lakini hukioni lina mpangilio wa maneno unaoonyesha kuwa pengine jibu litaanza na kiambishi ki-. Jibu ni kisogo

Umuhimu wa Vitendawili

(a)    Kutumbuza, kupumbaza na kuburudisha watoto hasa wakati wa jioni
(b)
   Kuhifadhi historian a utamaduni wa jamii
(c)
    Kama njia ya kuanzia, kukatizia au kumalizia usimulizi
(d)
   Huwa msingi wa kuyachambua maisha ya jamii
(e)
    Kuonyesha hisia za wanajamii kuhusu mtu au kitu fulani
(f)
    Kuelimisha kuhusu mazingira, imani, amali, mawazi na historia
(g)
    Kuchochea kufikiria kwa wanajamii kwa njia ya kupevusha kukabiliana na maisha yao
(h)
   Kukuza lugha kwa kuchangia katika kuiongezea msamiati
(i)
     Kudhihaki na kukejeli sifa na tabia zisizofaa
(j)
     Kukuza uwezo wa kukumbuka mambo muhimu na kujamii na kielimu
(k)
   Kuchochea udadisi na hamu ya kutaka kujua zaidi pamoja na utafiti
(l)
     Kukuza uhidari wa kusikiliza na wepesi wa kujibu maswali hivyo kuwatayarisha kukabili changamoto nyingi
(m)
Kutajirisha na kupamba mazungumzo
(n)
   Kujenga ari ya kushindana hivyo kujenga uhusiano mwema kati ya wahusika (mtegaji na mteguaji)
(o)
   Huwa hatua ya mwanzo ya ushairi

Aina za Vitendawili

(a)   Vitendawili sahili
Huwa na muundo rahisi wa maneno machache, aghalabu sentensi fupi hata neno moja. Huwasilishwa kama kauli wazi kuliko swali. Huwa na wazo moja. Mara nyingi hutegewa watoto.
Mifano ya vitendawili sahili ni pamoja na:
     (i)            Afuma hana mshale – nungunungu
   (ii)            Akikosekana maana imekosekana – kamusi
 (iii)            Akiona mwangaza wa jua hufa – samaki
 (iv)            Babu kasimama kwa mguu mmoja – uyoga / mwavuli
   (v)            Chauma bila meno, chaumiza bila ya silaha – moto
 (vi)            Dege kuu linainamia wanawe – nyumba
(vii)
            Fimbo yangu ndefu haina shina wala ncha – ulimwengu
(viii)
            Hata kama wataka kukitafuna hukiwezi, ni hafifu – maji
 (ix)            Hufa ukafufuka – bahari
   (x)            Nyumba yangu haina mlango – yai
(b)   Vitendawili Tata/ Changamano
Huwa kama fumbo refu. Huwa na wazo zaidi ya moja. Huhitaji kufikiri kwingi ili kupata jibu. Huwasilishwa kwa msamiati teule na maswali yaliyopangwa vilivyo.
Mifano ya vitendawili changamano ni pamoja na:
(i)
            Ana vichwa vitatu, miguu minane, masikio sita na mkia – watu wawili mgongoni mwa farasi
(ii)
            Mwenye miguu minne juu ya mguu minne akimsubiri mwenye miguu minne – paka juu ya meza akimngoja panya
(c)    Vitendawili Mkufu
Ni vitendawili ambavyo sehemu ya kwanza inahusiana moja kwa moja na sehemu ya pili kimuundo. Sehemu hizi mbili hujalizana na kuchangiziana.
Mifano ya vitendawili mkufu ni pamoja na:
     (i)            Nikitembea yuki, nikikimbia yuko, lakini nikiingia nyumbani hupotea – kivuli
   (ii)            Nikicheka kinacheka, nikinuna kinanuna – kioo
 (iii)            Nikienda pole huenda pole, nikikimbia hukimbia, nikiketi huketi – kivuli
 (iv)            Aliyekiona hakukikimbilia, aliyekikimbilia hakukiokata, aliyekiokota hakukila, aliyekila hakushiba lakini aliyeshiba hakufanya kazi yoyote – tumbo la binadamu na viungo vya mwili
   (v)            Aliyenunua hakutumia, aliyetumia hakuiona – sanda
 (vi)            Aliyechuma hakula, aliyekula hakumeza, aliyemeza hakushiba – mkono, kinywa na koo
(vii)
            Ukimwona Halima utasema ni Fatuma; ukimwona Fatuma utasema ni Halima – tui na maziwa
(viii)
            Ukiona ‘njigi’ utadhani ni ‘njege’, ukiona ‘njege’ utadhani ni ‘njigi’ –maziwa na tui la nazi
 (ix)            Teketeke huzaa gumugumu na gumugumu huzaa teketeke – mahindi ama yai
(d)   Vitendawili visimulizi
Ni vitendawili vinavyosimulia hadithi kama msingi wa kitendawili chenyewe
Mifano ya vitendawili visimulizi ni pamoja na:
     (i)            Kulikuwa na wasichana wawili waliokuwa wamesimama upande mmoja wa mto. Ng’ambo ya pili alikuwako baba yao na maembe mawili. Daraja lililokuwako mtoni lingemtoshea mwanamume mmoja na embe moja. Lakini lazima avuke mto huo na maembe yote mawili mara moja kwa ajili yao. Angefanya nini? – apande darajani na kuvuka akirusha maembe yake kwa zamu hadi avuke
   (ii)            Mtu alikuwa anakimbizwa na simba, akapanda juu ya mti. Juu kulikuwa na mzinga wa nyuki. Chini samba alimngoja. Mti huo ulikuwa karibu na mto. Ndani ya mto kuna mamba. Mtu huyu alikuwa na panga mkononi. Je, atajiokoa vipi? – atakata tawi la mti alitupe mtoni. Mamba atalikimbilia akidhani ni mtu Yule. Kisha mtu yule ataogelea majini avuke na kuenda zake salama
 (iii)            Nimeona mti wa ajabu; una mashina mawili na kila shina moja lina mizizi mitani; una matawi mawili na kila tawi lina majani matano – mtu
(e)    Vitendawili vya Tanakali
Huundwa kwa sauti za miigo fulani. Mifano ya vitendawili hivi ni pamoja na:
     (i)            Chubluu! – Jiwe liangukapo mchangani
   (ii)            Diii! Halina mshindo – Difu au ndifu
 (iii)            Drrrr! Hadi ng’ambo – Utandabui
 (iv)            Huku unasikia pa! Huku unasikia pa! – Mkia wa kondoo atembeapo
   (v)            Mti pakapaka! Mti haa! - zumari
 (vi)            Prrrrr! Hadi Makka – Utelezi
(vii)
            Tse! – Sindano mchangani (Kikamba)

Fani Katika Vitendawili

Lugha ya vitendawili huwa ya kitamathali. Baadhi ya tamathali katika vitendawili ni pamoja na:
(a)   Tashhisi
Vitu hupewa sifa za uhai kama wa binadamu. mifano ya vitendawili vya kitashhisi ni pamoja na:
     (i)            Askari wamekaa na mfalme yuko katikati – moto (mafiga yanalinganishwa na askari ambaye ni kiumbe hai)
   (ii)            Hana wema wowote – sumu
 (iii)            Atapanya mbegu nyingi sana lakini hazioti – mvua
 (iv)            Hamwogopi mtu yeyote – njaa
   (v)            Amefunika kote kwa blanketi lake jeusi – giza
 (vi)            Dadangu ana jicho moja – sindano
(vii)
            Ng’ombe wangu nisipomshika mkia hali myasi – uma, jembe au kijiko
(b)   Kwelikinzani
Kauli inayosemwainaonyesha ukinzani fulani kijuujuu lakini undani wake huwa hauna ukinzani huo. Pia huitwa ukinzani. Mifano ya vitendawili vya ukinzani ni:
     (i)            Aenda mbio lakini hana miguu – nyoka (tunatarajia anayeenda awe na miguu)
   (ii)            Ana meno mengi lakini hayaumi – shanuo au kitana (tunatarajia meno yaweze kuuma)
 (iii)            Ajenga ingawa hana mikono – ndege (awezaye kujenga tunatarajia awe na mikono)
 (iv)            Mwanamke hana mume lakini huzaa watoto wengi – mgomba wa ndizi (asiye na mume kawaida hazai)
   (v)            Nala lakini sishibi – mate
(c)    Takriri
Ni urudiaji wa maneno, sauti au vifungu fulani. Ifuatayo ni mifano ya vitendawili vinavyojumuisha takriri.
     (i)            Huona hapa, huko, huku na kule – kinyonga
   (ii)            Bak bandika bak banduka – nyayo (za mtu atembeapo)
 (iii)            Nikicheka kinacheka, nikinuna kinanuna – kioo
 (iv)            Amezaliwa Ali, amekufa Ali amerudi Ali – nywele
   (v)            Aliwa, yuala, ala aliwa – papa
 (vi)            Ganda mgando – ulimbo
(vii)
            Mti mnyama, mti kerekeche, mti ali, mti ali! – ngoma na upatu
(viii)
            Mahepe mahepe – magendo
(d)   Sitiari
Kitu kimoja hulinganishwa na kingine bila ya kutumia viungio. Ifuatayo vi mifano ya vitendawili vya kistiari.
     (i)            Popoo mbili zavuka mto – macho (macho kulinganishwa na popoo)
   (ii)            Gari la kila mtu – miguu (miguu kufananishwa na gari)
 (iii)            Embe langu la duara haliliki mpaka lipikwe – boga (embe linalinganishwa na boga)
 (iv)            Mhuni wa ulimwengu – nzi (kumfananisha nzi na mhuni

23 comments:

  1. mnashukuriwa kwa jitihada hii nzuri ya kukuza fasihi ya kiswahili.

    ReplyDelete
  2. Hongera! Kazi nzuri mmefanya. Endeleeni vivyo hivyo.

    ReplyDelete
  3. Napanda mti na kichaa wangu nini maana yake

    ReplyDelete
  4. Napanda mti na kichaa wangu nini maana yake

    ReplyDelete
  5. Hongera ingawa ninaomba majibu ya vitendawili hivi chalia chatembea na Chala chakula Cha mkononi,yakiwa hapa yapo pale

    ReplyDelete
  6. Booooring booooooooπŸ˜œπŸ˜œπŸ˜œπŸ™„πŸ™„πŸ™„πŸ™„πŸ˜‘πŸ˜‘πŸ˜‘πŸ˜‘

    ReplyDelete
  7. Blanketi langu Lina madoadoa....
    Ameukata mtu akauwacha ukitoa Moshi...
    Tap!tap! Tap! Pwaa!...
    Wazee wawili wanashuka mlima...

    ReplyDelete
  8. Kazi nzuri kweli. Tuzo mnalo langu.

    ReplyDelete
  9. ngumungumu kazaa legelege na legelege kazaa ngumungumu.....

    ReplyDelete