MWONGOZO WA MSTAHIKI MEYA
SEHEMU I
Onyesho I.
Mchezo uanzapo, tunakutana na Waridi ambaye ni nesi na Siki ambaye ni daktari. Wote wawili wako kwenye zahanati ya Jiji. Daktari Siki anaonekana mwenye kusumbuliwa na jambo fulani; pengine matatizo ya ukosefu wa dawa zahanatini.
Waridi aingiapo, wanaanza kuangazia swala la ukosefu wa dawa kwenye zahanati. Waridi anamwambia Siki kwamba, shehena ya dawa iko bahari kuu na kwamba ingewasili baada ya siku tatu. Hii ni kwa mujibu wa Mstahiki Meya mweneyewe. Zahanati ingepokea dawa hizo baada ya siku tatu zingine baada ya kuwasili nchini.
Meya anasema wagonjwa wasubiri dawa, naye daktari anashangaa kana kwamba ugonjwa nao utasubiri.
Kutokana na mazungumzo ya Waridi na daktari Siki tunagundua kwamba, zaidi ya kukosekana kwa dawa, wagonjwa hawana pesa za kulipia huduma za matibabu. Hata hivyo, amri ni kwamba, lazima wagonjwa walipie huduma za afya kabla hazijatolewa kwao. Waridi anatetea hali hii kwa kusema kwamba nchi yao ni maskini. Siki anapomuuliza mwenye kusema kwamba nchi ni maskini, Waridi anasema kwamba ameyasikia tu maneno hayo kutoka kwa wanasiasa, vyombo vya habari na wasomi. Siki haelekei kukubaliana naye na anashangaa kwamba ‘ameyasikia tu’. (Hii inadhihirishwa kwamba, vyombo vya habari, wanasias na wasomi wanawapotosha wananchi kwamba nchi yao ni maskini.)
Pindi anaingia mama mwenye mtoto mgonjwa. Waridi anamkemea lakini Siki anampokea na kuanza kumhudumia. Tunagundua kwamba, mtoto alikula maharage aliyoletewa na mamake kutoka anakofanya kazi; kwa Mstahiki Meya.Tunaonyeshwa hapa kwamba, jamii hii inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa chakula; haswa pale mama huyu anakiri kwamba huwa wanakula chakula cha mbwa bila ‘dhara yoyote’. Zaidi tunaona kwamba, mtoto huyu ana tatizo la utapiamlo; ushahidi wa kuwa pana ukosefu wa lishe bora.
Daktari anapendekeza mtoto alazwe kwenye wadi ya watoto na anajishughulisha kumpa huduma kwa kujitengenezea dawa ya mchanganyiko wa sukari na chumvi kwenye maji moto. Anapendekeza pia kwamba, wagonjwa wote waliolemewa walazwe hata ingawa hakuna dawa huku akisema kwamba wakifa watakufa kwa kukosa dawa lakini si kwa kukosa matumaini. Anasisitiza kwa kusema ‘ganga ganga ya mganga huleta tumaini.’
Tunapata kufahamu pia kwamba,wagonjwa hawa ni wafanyakazi wa Jiji husika.. dakatari anasema “…Asasi na wahudumiwa vyote viko chini ya Meya…” akiwa na maana kwamba, hospitali ni ya Jiji na wagonjwa ni wafanyakazi wa Jiji.
Inabidi wagonjwa walazwe huku dawa zikisubiriwa. Wakati uo huo Siki anashangaa ni kwa nini Meya akatoa kauli badala ya Bwana Uchumi na Kazi; inaelekea kuna jambo ambalo linaendelea pale na wanakubaliana kusubiri ili waone yatakayotokea.
Tathmini
Kutokana na onyesho hili tunaona kwamba, jamii hii imezingirwa na matatizo mengi: kwanza kuna tatizo la ukosefu wa dawa kwenye hospitali za umma. Pia kuna tatizo la ukosefu wa uajibikaji miongoni mwa viongozi kama vile Meya. Meya anatoa kauli ambazo hazifai kama vile kwamba ni lazima wagonjwa walipie huduma za afya kabla hazijatolewa kwao. Vile vile, kuna kutojali hali ya wananchi na haswa wagonjwa, wanatakiwa wasubiri dawa hadi zifike – ishara kwamba viongozi wao hawawajali. Waridi pia hawajibiki kazini mwake; anakuwa mkali kwa wagonjwa na pia anafuata kauli za wanasiasa bila kwanza kuzingatia maadili ya kazi yake: kuokoa maisha ya wagonjwa. Tatizo la njaa na umaskini linajitokeza wazi. Wananchi wanakula chakula cha mbwa na mabaki ya vyakula kutoka kwa matajiri.
Onyesho La Pili
Onyesho la pili latokea nyumbani kwa Mstahiki Meya. Yuko mezani huku mbele yake kukiwa na mayai na chai pamoja na vyakula aina aina. Sakafuni kuna zuliaya kupendeza. Mandhari haya ni ushahidi tosha kwamba Meya anaishi maisha ya hali ya juu nay a shibe ikilinganishwa na watu wengine Jijini. Tunamwona Meya akilalamikia ‘viyai’ alivyopewa. Mazungumzo yake yote yanaashiria mtu mwenye maringo, kiburi na kutojali. Yeye analalamika juu ya udogo wa mayai ilhali wengine hawana hata hayo mayai. Anmwagiza Dida amwagize mwenye kuleta mayai hayo asiyalete tena. Pindi anaingiadaktari Siki, nduguye. Huyu anamtabulisha Meya kwetu kwa jina Sosi. Meya haelekei kupendezwa na jambo ili; hataki kuitwa ndugu Sosi, maana eti yeye sasa ni Meya. Siki amekuja kwa Meya kumjulisha hali ilivyo kwa wananchi na haswa kuhusiana na ukosefu wa dawa na ukosefu wa fedha za kugharamia matibabu. Badala ya kutilia maanani maswala haya, Meya anajitia hamnazo na kuanza kusifu baraza lake kama baraza bora zaidi. Siki anamkosoa haswa kwa kujilinganisha na majirani dhaifu. Anapendekeza kuzingatia ubora zaidi ya ubora wa majirani zao. Anazidi kumsimulia Meya juu ya matatizo ya watu wao; anamwabia watu wanakufa kwa njaa na ukosefu wa mahitaji ya kimsingi. Anamtahadharisha juu ya kuwaongoza watu wenye njaa. Meya anasisitiza kwamba, wenye kumchagua ni wengi na watazidi kumchagua. Anamwambia Siki kwamba akili ni mali. Ili kuthibitisha hayo, anamwagiza Gedi kupeleka ujumbe unaoagiza idhaa ya baraza kucheza nyimbo za uzalendo kabla na baada ya vipindi maarufu. Siki anashangaa kama kwamba watu watashibishwa na nyimbo hizo na kusema kuwa, hamna haja kuwapigia watu nyimbo za uzalendo miaka hamsini baada ya uhuru. Siki analalamikia swala la maendeleo akisema, wanatembea lakini hawaendi mbele, waenda kinyumenyume. Anamkumbusha Meya kwamba, afya bora nay a bure kwa wananchi wote ni moja kati ya malengo ya mji katika mpango wake wa maendeleo ya miaka kumi. Meya anasema kwamba wao wako na malengo ya kimaendeleo ya millennia na kwamba huo ndio muhimu. Adadai kwamba wameshaingia katika kiwango cha kimataifa na kupinga hayo ni kama kumkama samba mwenye watoto. Siki anamkumbusha kwamba, kufikia kumi sharti kuanza na moja; kwamba kumi haifikiwi katika ombwe tupu (vacuum.) Meya anaudhika na kumwagiza Gedi kumtoa nje Siki. Kasha anaagiza asilikaribie jingo lake tena bali alione paa. Meya anaagiza kuwe na mkutano wa dharuru ofisini bila ya mwanakamati yeyote kukosa.
Tathmini
Onyesho hili linamwangazia Meya kama mtu asiyejali maslahi ya wananchi aongozao. Wao wana njaa naye ana shibe kuu kufikia kiwango cha kuangalia udogo na ukubwa wa mayai.
Hajali hali za watu wake, haswa juu ya umaskini, njaa na maradhi. Anapoambiwa kuna mtoto aliyekufa kwa njaa, anasema huyo ni mmoja na kwamba wamebaki wengi wanaomuunga mkono. Tofauti yajitokeza wazi kati ya ndugu wawili, Siki na Sosi. Siki ni mwenye utu ilhali Sosi ana ubinafsi mwingi na kiburi. Tofauti za kitabaka zinaonekana huku watu wa tabaka la juu wakiwa wanaishi maisha ya raha nao wa tabaka la chini wakiubeba mzigo mzito wa hali ngumu ya maisha; njaa na maradhi.
Onyesho La Tatu
Katika onyesho la tatu, madiwani watatu wako ofisini kwa
meya. Wameketi wakiwa wanamsubiri meya. Madiwani hao ni: kinara wa Masuala ya
Usalama, kinara wa Uhusiano Mwema, na wa Uchumi na Kazi.
Wamngojapo Meya, wanazungumzia maswala kadha; wanajadiliana
kuhusu hali ngumu ya maisha kwa wananchi. Diwani I na DiwaniII wanaonekana wazi
kutojali maslahi ya wananchi ilhali DiwaniIII anawatetea, pia ana maono.
Anasisitiza kwamba watu wanataka vitendo bali si maneno. Wenzake ambao ni
Diwani I na Diwani II waona kwamba, kuwepo kwao katika baraza ni bahati kubwa
na kwamba jukumu lao ni kulitetea Baraza la Mstahiki Meya.
Diwani III anawaambia wenzake kwamba, kuna kufaa na kujifaa,
akiwa na maana kwamba, baadhi ya madiwani wanatumia fursa yao kama viongozi
kujifaa badala ya kuwafaa waliowachagua.
Meya ajapo, anawapeleka moja kwa moja hadi kwenye ajenda ya
mkutano wao. Anasema kwamba, baadhi ya madiwani wanawachochea watu kuwa Baraza
limeshindwa kutimiza majukumu yake. Anadai kwamba, hata miongoni mwa walio
katika mkutano huo wao, wanawachochea wananchi.
Meya anwagiza kinara wa Usalama kuchukua hatua. Diwani I
ambaye ni kinara wa Usalama anamhakikishia kwamba atawaamrisha vijana wa
usalama (askari) kulilinda Baraza. Meya anmwambia kwamba mara hii hataki
kusikia mtu amekufa, anamwagiza Bwana Uhusiano Mwema kuhakikisha kwamba
ulimwengu haujui kwamba wanatumia askari kuwadhulumu wananchi.
Diwani I anaomba vijana kuandaliwa tamasha za nyimbo ili
kuimarisha uzalendo. Anasema watatunukiwa zawadi ndogo ndogo na kuonyeshwa
katika vyombo vya habari.
Diwani II –Bwana Uhusiano Mwema anatoa hakikisho kwamba
mashondano haya yatapeperushwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari ili
uzalendo uwamiminikie watu katika pembe zote za Cheneo.
Diwani III anasema kwamba, uzalendo hauji kwa watu kuimbiwa
nyimbo bali kwa kujibu vilio vyao. Analalamika kwamba watu hawana ajira, na
wale wenye ajira, hawapati mishahara ya kutosha. Pia wamelazimishwa na kaka zao
(wazungu) wanawalazimisha kupunguza idadi ya wafanyakazi. Pia wazungu hawa
hawajatoa hela za mkopo na kwa hivyo wafanyakazi hawawezi kuongezwa mishahara.
Anaendelea kusema kwamba watu wana njaa na wanahitaji dawa na dawa zenyewe
haziko. Tunakuja kufahamu kwamba dawa hizi haziji asilani.
Diwani III anendelea kusema kwamba ahadi za uwongo
zitachochea ari ya watu. Meya anasema wakigoma, watafutwa na wengine wasio na
kazi wataajiriwa.
Diwani II anapendekeza kuwe na kamati za kuhudumu ili
kupunguza joto la malalamiko. Diwani I anapendekeza madiwani wanaowaunga mkono
wawe viongozi wa kamati hizo.
Diwani II na Diwani I wanapendekeza nyongeza za mishahara
kwa walinda usalama na madiwani. Diwani III anapingwa kwa kusema kwamba hamna
fedha za kutosha. Pia anapendekeza madiwani walipe kodi kinyume na pendekezo la
Meya kwamba wasilipe. Hatimaye, Meya anaamuru madiwani wasitozwe kodi kwani
wana mzigo mkubwa wa kulihudumia Baraza.
Tathmini.
Katika onyesho hili, tuaona uozo ulioko katika Baraza.
Viongozi wengi wanajifikiria wao pekee huku wakitumia walinda usalama
kuwanyanyasa na kuwanyamazisha wananchi. Wafanyakazi hawapati mishahara ya
kutosha huku viongozi wakikataa kulipa kodi.
SEHEMU YA PILI
Onyesho La Kwanza
Onyesho hili linatokea ofisini kwa Meya. Meya anajiandaa kwa
mukutano wa mameya kutoka nchi za nje.
Katika maandalizi haya, anapanga kuwapa mapokezi ya kupigiwa
mfano. Watakaa katika hoteli ya kifahari na kula vinono. Mvinyo utaagizwa
kutoka Urusi na divai kutoka Ufaransa.
Rafiki yake, Bili, anamtembelea. Kutokana na mazungumzo yao
tunajua kwamba ni marafiki wa jadi, na kwamba, Bili ni mshauri wa Meya na ndiye
alimsaidia kufika alipo sasa.
Wazungumzapo pia, tunagundua kwamba mkewe Meya yuko ng’ambo
alikoenda kuwatemeblea wanawe na pia kujifungua mtoto mwingine. Wanawe Meya
wanasomea nje ya nchi kwa sababu viwango vya elimu vya huku kwao ni vya chini;
mkewe atajifungulia ng’ambo kwa kuwa wakunga wa huko ni wa hali ya juu
wakilinganishwa na wa huku kwao.
Swala la kandarasi linazuka ambapo Meya amefikishwa
mahakamani na mwanakandarasi kwa kutoheshimu mkataba. Bili anamshauri amhimize
mwanakandarasi kwenda mahakamani na akiri makosa yake ili Baraza limlipe fidia
kasha wagawane pesa hizo.
Waendeleapo na mazungumzo na mipango yao, zinasikika nje,
sauti za wafanyakazi wakilalamikia dhuluma na kusema wamechoka.anaarifiwa na
Gedi kwamba wafanyakazi wanadia mishahara zaidi naye Meya anatishia kuwafuta
kazi. Hatimaye anaamua kutafuta msaada kutoka kwa muhubiri.
Tathmini
Onyesho hili laonyesha uozo katika uongozi wa Jiji la
Cheneo. Viongozi wanajua viwango vya elimu na vya afya viko chini na badala ya
kuviinua, wanawapeleka watoto wao ng’ambo na kuwaacha wale wa maskini
wakiteseka. Mabibi zao wakitaka kujifungua wanapelekwa nje.
Onyesho La Pili
Onyesho hili latokea katika ofisi ya Siki. Mwanzoni,
tunamwano akiongea kwa simu na yaelekea anazungumza na Tatu –mmoja wa
wawakilishi wa wafanyakazi wa Baraza la mji.
Tena anjisemea mwenyewe kwa mtindo wa kishairi akisemwa
kwamba aliwaonya viongozi lakini hawakumsikia. Anasema kwamba, watu wenye njaa
wamewaangusha watu wengi wenye nguvu na madaraka.
Pindi Waridi anaingia na kumwarifu nia yake ya kujiuzulu na
kuacha kazi kwa vile haoni manufaa yake. Ameafikia uamuzi huu baada ya ya mtoto
wa mamake mdogo kufia mikononi mwake.
Siki anamshawishi asiache kazi kwa matumaini kwamba mambo
yatakuwa mazuri karibuni, pia kwa vile wagonjwa wanawahitaji, si kuwapa dawa
bali matumaini na kuwa pamoja nao hata ingawa kuwepo kwao hakuna tofauti na
vivuli vya wagonjwa wenyewe.
Tatu hatimaye anaingia na kueleza malalamiko ya wafanyakazi
na nia yao ya kususia kazi. Tatu analalamika kwamba wagonjwa wanakufa ovyo kwa
kukosa dawa na kwamba wamekuwa wakijaribu kukutana na Meya lakini kila mara,
diary yake huwa imejaa. Siki anaomba waendelee mbele hatua kwa hatua bila
kukata tama. Kasha Siki anawapa wazo la kutumia fursa ya wageni wajao mjini ili
kutoa rai yao kwa Meya. Anashauri wamwambie Meya kwamba hawatazingatia usafi wa
mji, na kwa vile anatarjia mameya kutoka miji mingine, huenda akasikiliza kilio
chao.
Tathmini
Wafanyakazi wamelemewa na mzigo mzito wabebeshwao na
viongozi wao. Hili huwa halina budi kutoke katika jamii yenye dhuluma. Tunaona
kwamba watu wenye njaa ni watu hatari kuongoza.
Onyesho La Tatu
Meya anaenda kwa muhubiri ili kuombewa. Tunamwona akiwa na
upole usio wa kawaida. Anapoombewa, askari wawili pamoja na Gedi wanaingia
ghafla na kuamuru kila mtu alale chini na kuinua mikono juu. Wanafanya hivi
bila kujua Meya mwenyewe yuko pale. Hii inaonyesha namna ambavyo askari hapa
wanawadhulumu wananchi wa kawaida. Wanapogundua kwamba Meya alikuwa pale,
wanaomba radhi na kusema kwamba, walisikia kelele na kudhani kwamba
vinyangarika walikuwa wanaleta vitina yao.
Hatimaye Meya anaomba msamaha kutoka kwa muhubiri. Kasha
anamwomba awe akipeleka maombi kwa Baraza mara moja kwa juma. Anaahidi kwamba,
mhubiri atakuwa akipewa pesa za petroli na kupata sadaka ya laki moja kila
mwezi.
Onyesho La Nne
Nyumbani kwa Diwani III(Bw. Kheri, Kinara wa Uchumi na
Kazi), Siki amemtembelea. Ameenda huko kufuatilia maswala kuhusu wafanyakazi na
matatizo yao.
Siki anamuuliza Kheri ni kwa nini hajamshauri Meya kutenda
mambo inavyompasa. Kheri anasema kwamba, amejaribu sana kumshauri Meya lakini
haelekei kumsikia. Anasema kwamba, Meya anakabiliwa na vikwazo mbalimbali;
amelewa na mamlaka na hasikii ushauri, kazungukwa na washauri wapotovu wenye
tama kubwa na njaa, Meya ana uwezo mkubwa vile vile, raia hawajahishwa katika
utatuzi wa matatizo ya uongozi.
Kheri anasema kwamba hatakata tamaa na ataendelea kumshauri
Meya. Pia anawalaumu wapiga kura kwani ndio huwachagua viongozi wabaya; anasema
kwamba, hata uchaguzi ukifanywa sasa, matokeo hayatakuwa tofauti sana. Anasema,
“…Mtu huvuna alichopanda…”
Siki anasema kwamba siasa ni
mchezo mchafu naye Kheri anasema kuwa anayeliogopa tope hawezi kujua
njia nzuri ya kulisafisha.
Maswala ya uongozi mbaya pamoja na unyakuzi wa ardhi
yanajitokeza hapa. Pia tunafahamishwa kwamba, Umeya hauna pato kubwa lakini
ofisi hiyo iko na mianya mingi ya kujipatia utajiri.
Harufu mbaya ya taka katika mji inasemekana kama kiwakilishi
cha uoz ulio ndani.
Tathmini
Katika onyesho hili, wahusika wawili waadilifu Dkt. Siki na
Bw. Kheri wanakutana. Kulingana na mazungumzo yao, ni wazi kwamba wanayafikiria
zaidi maslahi ya wananchi wa kawaida.
SEHEMU YA III
Onyesho I
Katika ofisi ya Meya.
Diwani III ameitwa na Meya ilii kupewa agaizo la kuwaongezea
madiwani mishahara. Zaidi ya kuwa wakati wa kuitayarisha mishahata umepita,
Diwani III anasema kwamba, hakuhusishwa katika kikao kilichoidhinisha ongezeko
hilo. Anaendelea kusema kwamba, wafanyakazi wamegoma kwa kutaka nyongeza ambayo
hawakupewa. Vile vile, uwezo wa baraza ni mdogo hivi kwamba kuwaongezea
madiwani mishahara kutaleta mivutano.
Meya anamlalamikia Kheri kwamba siku hizi haelekei
kukubaliana na jambo lolote siku hizi.
Meya anadai kuwajua wanaogoma na kwamba ana uzoefu mkubwa wa
mambo katika baraza na kungekuwa na vyeti hii leo angekuwa na Phd. Diwani III
anapendekeza wafanye kazi yao vizuri kwa minajili ya kesho na vizazi vijavyo.
Meya haoni hiki, alitakalo ni kuendelea kutawala na kunyakua mali. Anaamuru
madiwani wapewe nyongeza bila ya kujali malalamiko ya wafanyakazi.
Tathmini
Onyesho hili linaakisi mabavu yanayotumiwa na Meya katika
kuliendesha baraza. Anatumia nafasi mamlaka yake kutoa maagizo ya kuwapendelea
madiwani wenzake huku akiwapuuza wafanyakazi.
Onyesho II
Meya yuko ofisini mwake. Sauti za wafanyakazi zinasikika
wakidai haki zao. Kiongozi wao anawahutubia na kuwahimiza kudumisha umoja
katika kupigania maslahi yao. Mara inasikika milio ya risasi na vilio vya watu wakikimbilia
usalama wao. Meya anawacheka wafanyakazi kwa kutoroka. Bili, Diwani I na Diwani
II wanaingia na wanafanya mazungumzo pamoja na Meya kuhusu yaliyotokea.
Wanaelekea kulifurahia sana jambo lililotendeka la wafanyakazi kutawanywa na
polisi.
Wanapanga kusubiri siku tano hivi wawaone wafanyakazi
wakirudi kuomba kurejeshwa kazini. Diwani II anasema kwamba wawasukume
wafanyakazi hadi wajue kwamba wao ni wananchi na kuna wenye nchi.
Hawa wane, kwa kufuata ushauri wa Bili, wanapanga kuuza
Fimbo ya Meya iliyotengenezwa kwa dhahabu. Wanapanga kuuza Fimbo hii nje ya
nchi huku wakidai iliibiwa wakati wa fujo za wafanyakazi.
Tathmini
Katika onyesho hili, tunaonyeshwa namna ambavyo wafanyakazi
wanadhulumiwa kwa kupigwa na askari pindi wanapodai haki zao. Vile vile tunaona
viongozi amabao hawajali maslahi ya wafanyakazi. Zaidi ya yote, tunawapata
viongozi wawa hawa wakiiba raslimali za umma ili kujinufaisha wao weneyewe.
Onyesho III
Onyesho hili linaonyesha mhusika Dida ambaye anafanya kazi
kwa Meya. Anaigiza namna ambavy wafanyakazi walifurushwa na polisi pale
walipogoma. Anaanza maigizo yake kwa kusema: Duniani kuna watu na viatu
na cheneo ina watu na viatu
anamlinganisha mfanyakazi wa kawaida na askari na kusema
kwamba, askari na bunduki ni mfalme, ilhali mwenye kufagia anatukanwa na Bwana
na kudhalilishwa. Anakejeli hali katika Jiji la Cheneo na nama wazee walivy
otimua mbio hata kuliko vijana ili kuokoa nafsi zao.
Anakejeli zaidi na kusema kwamba, hayo yamhusu nini na bora
mameya wawepo ili apate watu kuwanadhifia nyumba.
Tathmini
Mwandishi anamtumia mhusika huyu kuikejeli hali ya mambo
katika Jiji la Cheneo. Anatupatia mtazamo wa mwandishi kuhusu uovu unaotokea
Cheneo.
Sehemu ya Nne
Onyesho I
Onyesho hili linafanyika ofisini mwa Meya, siku moja kabla
ya kufika kwa wageni. Meya anakutana na wawakilishi wa wafanyakazi. Wawakilishi
hawa wanatetea haki za wafanyakazi pamoja na nyongeza zao za mshahara.
Meya anashughulika zaidi na wageni wajao ilhali Baraza
halijaweza kuwalipa wafanyakazi wao waliogoma. Meya anawaomba wasubiri wamalize
na shughuli za kuwapokea wageni na waache kutoa vitisho. Wafanyakazi nao
wanataka kutumia nafasi hii ya kuja kwa wageni ili kuitisha nyongeza ya
mishahara. Wanatisha kutosafisha Jiji ili wageni wajapo wapate likiwa chafu na
lenye uvundo.
Wawakilishi wa wafanyakazi wanataka kushirikishwa katika
kikao cha Baraza ili watetee maslahi ya wafanyakazi lakini wanaambiwa hilo
haliwezekani.
Wawakilishi wa wafanyakazi wanasisitiza kwamba mgomo
utaendelea. Hawatashughulikia usafi wa Jiji na tishio la kipindupindu litakuwa
halisi.
Tathmini
Onyesho hili laonyesha msimamo wa wafanyakazi wa kupigania
haki zao pamoja na ule wa Baraza wa kutolegeza msimamo wake wa kuwanyima nyongeza
ya mishahara. Tokeo lake ni kuendelea kwa mgomo. Hali hii inaakisi hali halisi
katika mataifa mengi ya Kiafrika ambapo wafanyakazi wagomapo, hutishwa na
kusitiziwa mishahara yao.
Onyesho II
Ofisini mwa Meya, siku moja tangu mkutano na waakilishi wa
wafanyakazi. Meya anakutana na Diwani I na Diwani I. Meya analalamika kwamba,
mambo hayakwenda walivyopanga. Wafanyakazi bado wako mgomoni. Jiji limejaa taka
na harufu mbaya. Meya anaonekana
mwenye wasiwasi kwa kuwa mambo hayakwenda walivyopanga. Wageni wanatarajiwa
kufika siku hiyo ilhali wafanyakazi bado wamegoma. Kunatolewa pendekezo la
kutumia kipasa sauti kuwatafuta vijana wa kufanya kazi ya kusafisha mji.
Inatokea kwamba Bili ametoweka baada ya kumotosha Meya pamoja na madiwani
wenza. Meya anajilaumu kwa kukosa kumsikiliza Bwana Uchumi na Kazi. Mara habari
inafika kwamba wageni hawawezi kutwaa katika uwanja wao wa ndege na itabidi
watue katika mji jirani. Jambo hili
lilimkera Meya sana kwa sababu
Shuara ni mji mdogo tu, pia wageni
wanaogopa kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu. Tunaona kwamba mhazili
wa Meya naye achagoma.
Meya anaamrisha aitiwe askari lakini askari walikuwa
wanakuja kumjulisha safari ya wageni
imeahirishwa na na walikuwa wametumwa
kutoka makao makuu kumshika yeye Meya
pamoja na Diwani I na II ili wakaeleze
maana ya hali ilivyo Cheneo.
Meya, Diwani I na II wanawekwa pingu mikononi.
MAUDHUI NA DHAMIRA
Dhamira ni
funzo kuu litokanalo na kazi ya sanaa au lengo kuu la mwandishi.
Mwandishi wa
tamthilia hii anaangazia swala la uozo katika uongozi. Anashughulikia ukosefu
wa uwajibikaji wa viongozi katika jiji la cheneo.
Maudhui
Ubinafsi Kutowajibika
Umaskini Usaliti
Ufisadi Ulaghai
Unyanyasaji Migomo
Unafiki Mauti
Majuto Migogoro
Njaa Uzalendo
Uongozi mbaya Maradhi
Uozo Vibaraka
1. Uongozi mbaya
·
Ahadi za uongo kuhusu dawa.
·
Swala
la mishahara.
·
Viongozi
wanakataa kulipa kodi.
·
Hawasikilizi
maslahi ya watu.
·
Wanatumia
polisi kuwanyanyasa watu.
2. Ubinafsi
Hii ni hali ya mtu
kujifikiria zaidi ya watu wengine.
·
Watoto
wa meya wanasomea ng’ambo ilhali elimu katika jiji la Cheneo iko chini.
·
Meya
analalamika kuhusu viyai vidogo ilhali weungine hawana cha kukula.
·
Viongozi
wajiongeza mishahara.
·
Viongozi
hawalipi kodi.
·
Viongozi
wanafikiria kuhusu maslahi yao pekee.
3. Ufisadi
Ni hali ya kujipatia mali
kwa njia isiyofaa.
·
Meya
alikuwa amepelekwa kortini lakini Bili anamwonyesha jinsi watakavyoiba pesa za
mwanakandarasi.
·
Walinyakua
ardhi.
4. Njaa
Hali ya ukosefu wa chakula.
·
Watu
wanakufa kwa sababu ya njaa.
·
Mtoto
alifariki kwa kukosa chakula/ lishe bora.
5.
Maradhi
·
Watu
wanakufa kwa kukosa dawa.
·
Kuna
tishio la kuzuka kwa maradhi kama kipindupindu.
6.Umaskini
·
Kuna
ukosefuwa chakula dhidi ya umaskini.
·
Wagonjwa
hawana pesa za kulipia madawa hospitalini.
·
Watoto
hawasomi kwa sababu ya umaskini, hawana pesa za kulipa karo.
7.
Unyanyasaji/dhuluma
·
Watu
wanalipa kodi ilhali viongozi hawalipi.
·
Wafanyakazi
wanapogoma wanapigwa na askari.
8.
Unafiki
Hali ya mtu
kujifanya mzuri ilhali ni kinyume yake.
·
Meya
anaombewa na mhubiri na pia kumwahidi kumlipa.
·
E
Meya akizungumza na Bili anajifanya mzuri.
·
Anajifanya
mkarimu akishughulika wageni watakunywa nini.
9.
Kutowajibika.
·
Hawalipi
mishahara ya wafanyikazi.
·
Hawasikilizi
vilio vya watu.
10.
Migogoro
·
Mgogoro
dhidi ya meya na madiwani,viongozi dhidi ya viongozi.
·
Mgogoro
kati ya viongozi na raia inajitokeza kwa njia ya migomo/vitisho.
·
Meya
na nduguye Siki.
·
Kati
ya viongozi na wanataluma,ambapo viongozi wanataka kuwageuza kuwa wanasiasa.
11.
Uozo
Kuharibika
kwa mambo.
·
Wagonjwa
wanaacha hospitalini bila dawa.
·
Hali
iya watu kufa kwa njaa ilhali viongozi wanajifikiria wao wenyewe.
·
Viongozi
hawashughuliki na elimu ya watoto wa wananchi.
·
Meya
ananyakua viwanja vya ardhi na kuuza ili kujitajirisha.
·
Viongozi
wanapanga kuuza fimbo ya meya ya nchi.
·
Meya
anapotuma askari kuwachapa wafanyikazi wanapogoma.
12. Vibaraka.
·
Ni
wale watu ambao hufuata viongozi kwa upofu na kuwasifu hata wakifanya mabaya.kwa
mfano Diwani I na II.
13. Uzalendo
Hali ya mtu kuipenda nchi yake kwa dhati.
·
Diwani
III anatetea wafanyikazi na hakumbaliani na maamuzi yanayotolewa.Pia
analihurumia jiji.
·
Sili
anawahudumia wagonjwa na kuwatetea wafanyikazi.
14. Usaliti
·
Ni
kumtendea jambo ambalo ni kinyume kabisa na imani yake.
·
Meya
anasaliti jiji lake.
·
Viongozi
wanawasaliti wafanyikazi kwa kujiongeza mishahara.
·
Wanatekeleza
usaliti kwa;
-Kutoimarisha uchumi.
-Hawajaimarisha nafasi ya
ajira.
-Kuimarisha elimu na afya.
Badala yake wanafanya
yafuatayo;
·
Viwango
vya elimu na afya vyaenda chini na wao wanatafuta hizo nje ya ndani.
·
Wanajiongeza
mishahara mara kwa mara wanapokutana kwa kupora pesa za wananchi na kunyakua
ardhi.
15.
Ubadhirifu
Ni matumizi
mabaya ya pesa.
·
Wageni
wanapokuja wanapangiwa dhifa kubwa na kukaa kwenye hoteli ya bei ya juu na pia
kuagiziwa mvinyo kutoka nchi za nje.
·
Wanaomba
marupurupu na meya anakubali.
·
Meya
anapanga mhubiri awe anapewa pesa kila mwezi ili kumvutia.
·
Madiwani
wanaongezwa mshahara kiholelaholela.
16. Usugu
Ni hali ya
mtu kusikia wala kukubali ushauri.
·
Meya
amejaribiwa kuzungumziwa na Sili ilhali anakataa kuyasikia anayosema.
17.
Majuto
Ni
masikitiko kwa jambo ambalo limetokea.
·
Diwani
I na II wanajuta kwa kukubaliana na Meya kuleta uozo katika jiji la Cheneo.
18.
Ulaghai
Hali ya kumnyang’anya
mtu mali kwa kuutumia ujanja.
·
Meya
anawaongezea viongozi mishahara ilhali wafanyikazi wanadai kuongezwa mishahara
lakini Meya anawaambia kuwa hakuna pesa.
19.
Migomo
·
Ni
hali ya wafanyikazi kukataa kufanya kazi hadi masharti fulani yatimizwe.
·
Wafanyikazi
walipogoma wakidai kuwa waongezwe mishahara yao .
20. Mauti
Ni hali
inayomfanya kiumbe kukosa uhai.
·
Wakati
ambapo mtoto wa mamake mdogo Waridi alikufia mikononi mwake.
·
Tatu
alipokuwa analalamika kuwa wagonjwa wanakufia hospitalini kwa kukosa dawa.
WAHUSIKA
1.Meya
Sosi
Ndiye Meya
wa jiji la Cheneo.
Ni ndugu
wa daktari Siki na rafikiye Bili.
Sifa zake
1. Ananyakua ardhi
Ni mwizi-alikuwa amepanga
kuiba fimbo ya Meya na kuiuza.
2.Ni mwenye ubinafsi.
Anajifikiria yeye
mwenyewe, analalamika kuwa viyai ni vidogo, ilhali wengine hawana chakula.
Wanajiongeza mishahara
lakini hawaongezi mishahara ya wafanyikazi.
3.Ni msaliti.
Amewasaliti wananchi kwa
kutowajibika katika kazi yake ya uongozi.
4.Ni mtu sugu.
Kwa kuwa hafuatilii
ushaurianaopewa na nduguye Siki.
5.Ni Mlaghai.
Amenyakua ardhi na kuiuza
kwa manufaa yake mwenyewe.
6.Ni mwenye majuto.
Anajuta kwamba mambo
yanakwenda kinyume na alivyotarajia.
7.Ni mnafiki.
Anajifanya mwema kwa
mhubiri na kutoa sadaka kanisani ya laki moja.
8.Ni mwongo kwani
anadanganya kuwa dawa ziko ilhali hakuna.
9.Hana utu
Hii ni kwa sababu
alipoambiwa kuwa motto mmoja alikufa hakujali na kusema kuwa ni mmoja tu.
10. Ni mnyanyasaji.
Wafanyikazi wanapogoma,
anatumia polisi kuwapiga wananchi.
11. Ana upeo finyu.
Haoni mbali.Hakufikiria
jinsi mambo yatakavyoenda mrama.
12. Ni mtovu wa
uzalendo.
Hashughuliki na
wafanyikazi na taasisi ya elimu ya jiji la
Cheneo.
13.Ni mtu mjinga,
Alidanganywa na Bili hadi
mambo yanakwenda mrama.
14.Ni mtu mwenye
majivuno.
Hawezi kula vile viyai
vidogo.
Umuhimu
·
.Ni
kielelezo cha upotovu katika jamii.
·
Anaonyesha
ubinafsi na mivutano na kutowajibika miongoni mwa viongozi.
·
Kupitia
kwake tunaona mwandishi akionyesha uongozi mbaya.
2 .Diwani
III
Sifa
1.Ni
mwadilifu.
·
Ni
mtu mwenye maadili mwema.
·
Anapinga
mambo mabaya ya Meya.
2.Ni
mnyenyekevu.
·
Alidumisha
heshima ya Meya ingawa alijua kuwa ni mwizi.
3.Ni mtu
asiye na tamaa.
·
Hana
tamaa ya kuongezwa mshahara na anapinga baadhi ya uamuzi unaofanywa na wengine.
4.Ni
mzalendo.
·
Anawashughulikia
wananchi na anataka viongozi wenzake walipe kodi.
5.Ni
mwenye subira.
·
Amemshauri
Meya lakini haonyeshi mabadiliko.
6.Ana ushauri
mwema.
Umuhimu.
1.Ni mpinzani
mkubwa wa maovu katika jamii.
3.MadiwaniI na II.
·
Ni
mabarakala wanaotenda mambo ili kumfurahisha Meya Sosi.
·
Ni
mwenye tamaa.Wanataka nyongeza ya mishahara bila kujali wananchi na wanakataa
kulipa kodi.
·
Wanapenda
mizengwe(mipango ya kisirisiri)bila kumhusisha diwani III
·
Ni
waongo.Wanawadanganya wananchi juu ya madawa na kuhusu nchi.
·
Ni
watu wenye njama.Wanapanga kuuza fimbo ya Meya.
·
Hawana
msimamo imara.Hawashikilii mambo,wanafuata amri za Meya bila kuuliza maswali.
·
Ni
wajinga.wanasaliti wananchi waliowachagua.
4.Siki.
Ni daktari katika zahanati
ya jiji la Cheneo.
Sifa
1.Ni
mwadilifu-anawashughulikia wananchi.
2.Ni mwenye bidii.
3.Mwenye ushauri nasaha.
4.Mtulivu.
5.Ni mtu mbaraza.
6.Mkereketwa.
5.
Bili
Ni rafiki
yake Meya.
Sifa
I.Ni mbunifu
2.Ni mjanja
3.Ni mpotovu
4.Ni mwenye tama
5.Ni mnafiki
6.Tatu
Ni mwakilishi wa
wafanyikazi.
Sifa
1.Ni mtetezi mkali wa haki
na maslahi.
2.Ni jasiri.
3.Ni mbaraza.
4.Ni mnafiki.
Mtindo na matumizi ya
lugha
1.Kinaya.
2.Methali.
3.Sajili ya dini.
4.Kuchanganya ndimi.
5.Tashbihi.
6.Semi.
7.Uzungumzi nafsia.
1. Kinaya.
Ni hali ya mambo kutokea
kinyume na matarajio.
Mfano:
·
Tamthilia
hii inaonyesha kinaya wakati ambapo Meya alikuwa anawaambia wagonjwa wasubiri
dawa eti kwamba zitakuja baada ya siku tatu ilhali hakuna dawa zozote.
·
Kinaya
kinajitokeza tena pale ambapo meya anajifanya mzuri kwa mhubiri anapoenda
kumwomba msamaha.Pia anaahidi kuwa mhubiri atakuwa akipewa pesa za petroli na
kupata sadaka ya laki moja kila mwezi.
·
Pia
tunaona kinaya katika tamthilia hii wakati ambapo Meya alikuwa anateta kuhusu
viyai vidogo ilhali wengine katika jiji la Cheneo hawana chakula.
2.Methali
Ni kifungu cha maneno yanayotumiwa pamoja
kisanii kwanjia ya kufumba au kupigia mfano.
Mifano:
1.Ngoja
ngoja huumiza matumbo.
·
Hii
methali inatumiwa katika hadithi hii kueleza kwamba jambo linalostahili
kutendwa papo hapo lisipotendwa kwa wakati ufaao,hutia hasara.
·
Methali
hii ilitumiwa na Siki wakati ambapo alikuwa akimweleza Waridi kuwa wagonjwa
wanasubiri dawa ziwasili,ugonjwa nao hautasubiri.
2.Haraka
haraka haina Baraka.
·
Maana
ya methali hii ni kuwa jambo lifanywalo haraka haraka haliwezi kufana,sharti
liende kwa mpango wa taratibu.
·
Methali
hii ilitumiwa na Waridi kumwambia Siki huwa asiwe na haraka ya kuwashughulikia
wagonjwa kwani hawana hela za kulipia huduma za zahanati.
3.Dawa ya
adui ni kummegea unachokula.
·
Methali
hii ilitumiwa naBili kwa Meya juu ya kugawana fidia baada ya mwanakandarasi
kuishtaki Baraza.
4.Wasemao
mchana usiku watalala.
Maana;watu
hata wakisema itafika wakati wachoke.Bili anaitumia methali hii kwa kurejelea
sauti za wafanyikazi wanaogoma.
5.Ganga
ganga za mganga huleta tumaini.
Kurukaruka
kwa mganga huletea wagonjwa tumaini.Siki anaitumia methali hii kwa Waridi ili
awaletee wagonjwa matumaini.
6.Mbiu za
sakafuni huishia ukingoni.
Ina maana kuwa mambo yaliyofanywa kwa giza
yatafichuliwa.Bili anatumia kurejelea kwa wanahabari wanaotaka kuhoji Meya
kuhusu mgomo.
7.Asante
ya punda ni mateke.
Maana ya
methali hii ni kuwa ukifanya mtu mema anakulipa na maovu.Meya anaitumia methali
hii kwa mhazili wake aliyeacha kazi.
8.Msiba wa
kujitakia hauna kilio.
Ina maana
kuwa ukijiletea shida hauna mtu wakulaumu ila wewe mwenyewe.
9.Yaliyopita
yamepita tugange yajayo.
Hii methali
ina maana ya mambo yaliyopita yamepita tungoje yajayo.
10.Mpiga
ngumi ukuta huumiza mkonowe.
Hii methali ina
maana kuwa ukifanya mambo ukidhani unawaumiza wengine,wajiumiza wewe mwenyewe.
MBINU YA
KUCHANGANYA NDIMI.
Hii ni hali
ya kutumia lugha nyingine isipokuwa lugha yenye hadithi imeandikwa nayo. “What
do you think this is?food poison.
·
”Ooh
yes”I understand.
·
“Collective
responsibility.
·
“Yes
sir”(Gedi).
Tashbihi.(pg 47,48,45,14,34,69).
Hali ya
kulinganisha vitu na maneno ya ulinganishi kama vile kama,mithili ya.kwa mfano;
·
Kumkunja
kila aliye chini yake kama ua wakati wa alasiri –Diwani wa III ndiye aliyenena haya
kwa siku kuwa Meya ana uwezo.
·
Ni
kama mtoto na chakula-DiwaniIII ndiye aliyenena haya kwa Siki kumwonyesha kuwa
cheo kinaweza levya mtu asahau alipokuwa jana.
·
Kushindana
naye ni kama kushindana na ndovu-Diwan III aliyanena haya kwa Siki kumwonyesha kuwa
Meya ana mamlaka makubwa.
·
Inasimama
kama ya mtende –Ni Siki aliyoyasema maneno haya
kwa Diwani III kwani hakutarajia kumpata kwake na bahati yake
akailinganisha nay a mtende.
Mimi na Menga ni mfano wa mfano wa mafuta na maji-Siki
anamweleza DiwaniIII kuwa yeye na Meya ni mfano wa mafuta na maji,kwani
hawajali kubaliana kwa maswala mbalimbali.
·
Kumpiga
haya ni sawa na kumkama simba mwenye watoto.Haya ni maneno ya Meya aliyoyanenea
Daktari Siki kuwa akipinga malengo ya kimaendeleo ya milenia ni hatari kwani ni
kama kumkamua samba mwenye watoto.
·
Amekufa
kama nzi-Beka ndiye aliyenena maneno haya kwa Meya;kifo cha mtoto wa Kerekecha
alikufa kililinganishwa na kifo venye nzi hufa ovyo.
Misemo.
Mifano.
·
Watu
sasa wanatumbua mbivu na mbichi-Huu msemo ulinenwa na DiwaniIII kwa DiwaniI na
DiwaniII kuwa hakuna geni ambalo watawaambia watu kwani wanayafahamu yote.
·
Ndiyo
huko kuwaua ndege watatu kwa jiwe moja.Huu ni msemo wa Meya kwa Bili ambapo
Bili kamwambia kuwa kandarasi mpya yategemea kauli yake.
·
Msikate
tamaa-Huu ni msemo wa Siki kwa Tatu kuwa wasikate tamaa kushinikiza kumwona
Meya.
·
Aliyeliogopa
tope kummwangikia hawezi kujua njia nzuri ya kulisafisha-DiwaniIII ndiye
aliyesema msemo huu kwa Siki.
Mdokezo.
Ni mbinu ya kukatiza
msemo.
Km.Amesema mwenyewe
Meya….Haya ni maneno ya Waridi kwa Siki akimweleza kuwa dawa zaja.
Na leo…Afadhali jana.Haya
ni maneno ya mama mwenye mtoto mgonjwa kwa Siki kumweleza hali ya mtoto wake.
Lakini daktari ha…Haya
maneno ya Waridi mama kwa Siki kumwambia mama mwenyewe hana pesa za kulipia
huduma zao.
Hata huhitaji wakili…Haya
maneno ya Bili kwa Meya kuhusu ile kesi ya mwanakandarasi.Ni kama…..ni
kama…Talk of devil…Haya ni maneno ya Bili kwa Meya.
Lililoandikwa….Haya ni
maneno ya DiwaniIII kwa Siki.
Ni…ni…ni…Haya ni maneno ya
Gedi akitaka kumwarifu Meya habari kuwa wanauwanja wamegoma.
Sitiari/Jazanda
Kwa mfano.
·
Unamkanya
nyoka mkia.
Maneno haya yalisemwa na
Siki akimwambia Meya kuhusu mambo yangemgeuka na kuharibika kwa
kutowashilikisha watu katika mipango ya baraza.
·
Watu
sasa watafahamu mbivu na mbichi.
Maneno haya yalisemwa na
DiwaniIII akiwaambia madiwani wenzake kuwa watu wanayaelewa mambo sasa.
·
Lazima
kwanza mnihakikishie kuwa huyo sumu hapati hata tununu ya mambo hii.Hii ni bomu
inaweza kutulipukia usoni.Maneno haya yalisemwa na Meya kwa DiwaniI na II
wakati walipotaka kuiuza fimbo ya Meya.
Uzungumzi nafsi.
Hali ya mtu kuzungumza
pekee/nafsi yake.km.
i)Dida.
-Anazungumza juu ya kazi
ya askari.
Jambo la watu kukimbia
mbio.
ii)Meya.
Baada ya mazungumzo na
DiwaniIII anabaki kusema peke yake.(uk56)”….Nifikiri ninaweza kusikiliza
viongozi wao si kila mtu!”
Tashtiti.
Mbinu ya kutumia
vichekesho au dhihaka ili kufichua uovu Fulani.km
·
Kuna
watu na viatu-Dida anaeleza uovu katika cheneo namna ya dhihaka.
·
Meya
kutamka maneno ya kidini-Mwandishi anatumia njia hii kuashiria jambo fulani
kama unafiki.
·
Daktari
anatengeneza mchanganyiko wa maji ,sukari na chumvi.Anaonyesha mambo
yameharibika kabisa.
·
Meya
na marafiki zake wanashikwa na polisi-wakikuwa na mamlaka makubwa.
NAMNA YA KUJIBU MASWALI YA
FASIHI.
Kuna maswali ya aina mbili
katika fasihi;
-Maswali ya muktadha.
-Maswali ya insha.
a)Maswali ya muktadha.
Swali la muktadha
huhusisha dondoo kutoka kitabuni ambapo mtahiniwa hutakiwa kuiweka dondoo hilo
katika muktadha wake.Muktadha hapa ina maana ya mazingira ya kutokea kwa
jambo.Katika kulijibu swali la muktadha mambo manne huhusishwa.
i)Mwenye kuyasema.
ii)Mwenye kuyambiwa.
iii)Mahali walipokuwa.
iv)Swala lenye lililokuwa
likiendelea.
Km.Wewe wa ndani zaidi
kuliko mimi…kama ni habari utakuwa unazipata kwa urahisi kuliko mtu wa nje…
Mwenye kuyasema maneno
haya ni DiwaniIII.Alikuwa anamwambia Siki.Walikuwa nyumbani mwa
DiwaniIII.Walikuwa wanazungumzia venye watamwona Meya kutetea maslahi ya watu
wa Cheneo.
b)Maswali ya insha.
Maswali haya yanazingatia
mpangilio wa aya.k.m.Taja na ufafanue maudhui kumi katika tamthilia ya Mstahiki
Meya.
·
Utangulizi-Uwe
mfupi wa kilenge moja kwa moja.km.katika tamthilia hii ya Mstahiki Meya.
Ingawa ninampa mwenye fikra hii mkono wa Tahania ,ningependa mhusika wa hiki kifungu hiki azidikuujenga hadi Mwisho wa Mstaki Meya!...
ReplyDeleteShukrani Gallic Thomz. Mwongozo huu utakamilika hivi karibuni.
Deleteshukrani
ReplyDeleteKaribu Santa Mariah
DeleteThis comment has been removed by the author.
ReplyDeleteJe,unaweza kunieleza kwa ufaafu anwani hii'Mshtahiki Meya'?
ReplyDeleteanwani ya mstahiki meya ni kinaya jadili
ReplyDeleteSHUKRAN ZIKUFIKIE
ReplyDeleteAsante. Mwongozo wa Kidagaa Kimemwozea waandaliwa.
ReplyDeleteHeko wadadisi wa lugha kwa kazi murwa
ReplyDeleteshukran'
ReplyDeleteasante
ReplyDeleteKazi nzuri hii inapendeza. Shukran'
ReplyDelete